Who we are



 

Bohari kuu ya Dawa Zanzibar ni moja kati ya taasisi za Wizara ya Afya yenye jukumu la kupokea, kuhifadhi na kusambaza Dawa muhimu, Vifaa tiba, Vifaa vya uchunguzi wa Kimaabara na uchunguzi wamionzi. Mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitangaza Sera ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wote bila ya malipo. Miongoni mwa maeneo muhimu ya huduma hizo ilikuwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa za afya. Usimamizi wa huduma hizi uliwekwa chini ya Idara tofauti zikiwemo Idara ya Mipango na Uendeshaji, Idara ya Tiba na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu katika Wizara iliyohusiana na Afya.

 

Mnamo mwaka 2008 Serikali ilitunga Sera ya Dawa iliyopelekea kuanzishwa Idara ya Mfamasia Mkuu wa Serikali ambapo Bahori ya Dawa ilikuwa sehemu ya Idara hiyo. Idara ilipewa, pamoja na mambo mengine, jukumu la usimamizi wa dawa, vifaa tiba na bidhaa za afya kwa hospitali na vituo vya afya vya umma. Katika kutekeleza majukumu yake, kati ya mwaka 2008 hadi 2012, Idara ilitekeleza Mpango wa Majaribio wa Kupeleka Dawa, Vifaa tiba na Bidhaa za Afya Kulingana na Mahitaji ya Kituo (Pull System) uliochukua nafasi ya utaratibu wa awali wa Kupeleka huduma hizo bila ya kuzingatia mahitaji yao (Push System). katika kuongeza ufanisi wa huduma za dawa nchini, mwaka 2011 Bohari ilipandishwa hadhi kuwa Idara kamili na kupewa jukumu la kupokea, kusimamia, kuhifadhi na kusambaza dawa, vifaa tiba na bidhaa za afya.

 

Mwaka 2012 Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) ilijenga jengo jipya la Bohari lenye ukubwa wa mita za mraba 1,025 katika eneo la Maruhubi, Unguja. Ukubwa huu unaiwezesha Bohari kuhifadhi kiasi cha marobota (pallets) 580 ya dawa kwa wakati mmoja. Kwa upande wa Pemba, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global Fund) imejenga jengo jipya la Bohari katika eneo la Vitongoji lenye ukubwa wa mita za mraba 914 na uwezo wa kuhifadhi marobota 515 ya dawa kwa wakati mmoja. Pamoja na kuweko kwa miundombinu hii, Utaratibu wa ununuzi wa dawa, vifaa vya tiba na bidhaa za afya bado unaendelea kufanywa na Wizara ya Afya kutokana na Bohari kutakuwa na uwezo kisheria kutekeleza jukumu hilo.